Tuesday, May 19, 2015
MAWAZIRI wa Afrika Mashariki kutoka nchi tano za Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), walikutana jana kwa saa 1:08 asubuhi jijini Arusha
kujadili hali ya uchaguzi nchini Burundi kutokana na maazimio matatu.
Miongoni mwa maazimio hayo ni kuitaka Tume ya Uangalizi ya Uchaguzi
wa Burundi kutoka nchi za EAC, inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba
kuendelea na kazi hiyo nchini humo mara moja.
Aidha, imeazimiwa kuwa, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, Dk
Harrison Mwakyembe na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya EAC, Dk Richard Sezibera
kutembelea Burundi mapema iwezekanavyo kwa lengo la kujionea hali
halisi katika nchi hiyo.
Kikao hicho cha dharura kilichofanyika makao makuu ya EAC jijini Arusha
kuanzia saa 6:12 mchana na kumalizika saa 7:24 mchana huo kikiwa chini
ya uenyekiti wa Dk Mwakyembe, kilihudhuriwa na karibu mawaziri wote
wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, isipokuwa, Valentine
Rugaine wa Rwanda ambaye haikuelezwa sababu za kushindwa kushiriki.
Dk Sezibera alizungumza na wanahabari na kusema moja ya mambo
yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kupokea taarifa ya kikao
cha wanasheria wakuu wa nchi za EAC, kilichofanyika mwishoni mwa wiki
jijini hapa.
“Baraza la mawaziri limepokea taarifa ya kikao cha
wanasheria wakuu wa nchi za EAC kilichokuwa na lengo la kujadili hali ya
Burundi.
“Taarifa hii iliyowasilishwa itakabidhiwa kwa wakuu wa nchi za EAC
katika mkutano wa makuu hao unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni,”
alisema.
Kwa mujibu wa Dk Sezibera baraza hilo la mawaziri, liliazimia mambo
makuu matatu, ikiwa ni pamoja na Tume ya Jaji Warioba kuendelea na kazi
hiyo nchini Burundi, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC na Katibu
Mkuu wa Jumuiya hiyo kutembelea Burundi, huku mawaziri wa EAC wakipewa
jukumu la kutembelea kambi za wakimbizi zilizopo Rwanda na Tanzania kwa
lengo la kujionea hali halisi ya maisha ya wakimbizi katika kambi zote
zilizopo katika nchi hizo.
Awali, Waziri anayeshughulikia Afrika Mashariki kutoka Burundi,
Leontine Nzeyimana aliwataka wananchi wa Burundi kuwa watulivu katika
kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Aidha, aliwataka wananchi hao kutambua kuwa Burundi ni mali yao na
hawana nchi nyingine, hivyo ni vyema wakawa na subira kwa kuwa uchaguzi
upo pale pale.
Kikao hicho cha dharura ni mwendelezo wa vikao vya kutafuta suluhu ya
machafuko ya kisiasa, yanayoonekana kuinyemelea Burundi hasa baada ya
Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa awamu ya tatu katika
uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Uamuzi huo unapingwa na makundi kadhaa na wiki iliyopita Nkurunziza alinusurika kupinduliwa na mahasimu wake.
No comments:
Post a Comment