Tuesday, June 9, 2015

Jack Warner alia Marekani inalipa kisasi

Aliyekuwa makamu wa rais wa shirikisho la Soka Duniani FIFA, Jack Warner
Aliyekuwa makamu wa rais wa shirikisho la Soka Duniani FIFA, Jack Warner, ameituhumu Marekani kwamba inafuatilia mashtaka ya rushwa dhidi ya maafisa waandamizi wa shirika hilo kwa sababu imeshindwa kuwa mwenyeji wa kombe la dunia la mwaka 2022.

Akiandika katika gazeti ambalo analolimiliki huko Trinidad na Tobago, bwana Warner amesema tuhuma hizo dhidi yake na wengine kumi na tatu zinaonyesha kwamba Marekani inaegemea upande mmoja.
Warner amekana tuhuma hizo. Shirikisho hilo la Soka Duniani limegubikwa na tuhuma za rushwa kwa kipindi cha wiki mbili mfululizo. Akiandika katika gazeti lake linaloitwa Sunshine, Warner anaelezea mashtaka ya Marekani dhidi yake kuwa ni uonevu na yaliyoegemea upande mmoja.
Warner amesema Marekani ambayo inajifanya kuwa ni polisi wa dunia, imehamasika kuchukua hatua hiyo baada ya kushindwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2022.Warner, mwenye umri wa miaka 72 amekana tuhuma za kupokea rushwa ya dola milioni kumi za kimarekani kutoka Afrika Kusini baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2010.
Katika makala yake, Warner ameendelea kujitetea kwa kusema kuwa, kuishutumu Afrika Kusini kunachafua hadhi ya hayati Nelson Mandela ambaye ameisaidia Afrika Kusini kupata nafasi hiyo.
Gazeti hilo limeonyesha picha za Jack Warner akikutana na Prince William, David Beckham, Barack Obama na Vladimir Putin ambao amesema wote walikuwa na ushawishi pindi nchi zao zilipokuwa zikifanya kampeni ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia.Jack Warner amemalizia kwa kuuliza iwapo walikuwa wanatumia takrima kama rushwa?
Jack Warner ni mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa bodi ya shirikisho la soka duniani FIFA, ambao wanatuhumiwa kwa kashfa ya rushwa na mpaka sasa Warner amekana tuhuma zote zinazomkabili.

No comments:

Post a Comment