Monday, April 13, 2015
wapendao blog
Watu 18 wamekufa papo hapo kwa kuteketea kwa moto na wengine 11 wamejeruhiwa vibaya kutokana na basi walilokuwa wakisafiria kugongana na lori aina ya Mitsubishi Fuso, katika kijiji cha Msimba tarafa ya Mikumi, barabara kuu ya Morogoro – Mbeya.
Ajali
hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Nganga linalofanya safari zake
kutoka Wilaya ya Kilombero kuelekea mkoani Mbeya na kugongana na lori
hilo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alisema ajali hiyo ilitokea
jana saa mbili asubuhi katika eneo hilo huku likihusisha basi aina ya
Scania lenye namba za usajili T373 DAH na Fuso lenye namba za usajili
T164 BKG.
Alisema
chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi la Nganga ambaye alikuwa katika
mwendo kasi na kulipita gari lililokuwa mbele yake bila ya tahadhari na
kukutana na lori hilo na kisha kugongana nalo katika eneo hilo.
Alisema
baada ya magari hayo kugongana, ndani ya buti ya basi kulikuwa
kumepakiwa pikipiki ambayo ilikuwa na mafuta na baada ya kutokea ajali
hiyo kulitokea mlipuko wa moto na kusababisha basi hilo pamoja na lori
kuwaka moto.
Kamanda
huyo alisema kuwa kutokana na moto huo, baadhi ya abiria waliokuwepo
katika basi hilo walishindwa kujiokoa na hivyo miili yao kuteketea
kabisa na moto huo, wakiwemo madereva wote wa magari hayo.
Alisema
majeruhi 11 wa ajali hiyo wamekimbizwa katika Hospitali ya Mtakatifu
Kizito iliyopo tarafa ya hiyo Mikumi kupatiwa matibabu huku hali zao
akieleza kuwa baadhi yao ni mbaya kutokana na kuungua vibaya kwa moto.
Kamanda
huyo alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali hiyo
ambapo mpaka sasa haijatambulika majina yake, licha ya madereva wa
magari yote kufa.
Hata
hivyo, Kamanda huyo alishindwa kutaja majina ya majeruhi kutokana na
baadhi yao kuendelea kupatiwa matibabu kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Naye
Mganga wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi, Dk Boniventure
Buyagabuyaga, alithibitisha kupokea jumla ya miili ya marehemu 18 ambao
walikuwa wameteketea vibaya kwa moto kutokana na ajali, ambapo alisema
tayari imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhiwa maiti kwa ajili ya
kusubiri utambuzi.
Alisema
mpaka sasa majeruhi wanaotibiwa katika hospitali yake wamebaki saba,
lakini hali zao bado ni mbaya kutokana na kuungua moto katika sehemu
mbalimbali za miili yao.
Ajali
hiyo imekuwa sawa na mwendelezo wa ajali za mabasi nchini, kwani
Alhamisi iliyopita watu 12 walikufa katika ajali zilizotokea Tanga na
Morogoro, huku wengine wanne waliokuwa wakisafiri kwa basi la Nyehunge
wakiaga dunia usiku wa Jumamosi mkoani Dodoma.
Katika
ajali iliyotokea mkoani Tanga, katika kijiji cha Mbweni Mkata, majira
ya asubuhi, ilihusisha basi la Kampuni ya Ratco ya Tanga liligongana uso
kwa uso na basi la kampuni ya Ngorika na gari dogo aina ya Toyota Passo
na kusababisha vifo vya watu 10 papo hapo, akiwemo mmiliki wa gari
dogo, Musa Lupatu aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Korogwe Vijijini.
Katika
tukio la Morogoro, watu wawili walikufa na wengine 48 kujeruhiwa katika
ajali iliyosababishwa na basi la Happy Nation lililokuwa likitoka Dar
es Salaam kwenda Mbeya na kupata ajali eneo la Mikumi.
Aidha,
Machi 12, mwaka huu mkoani Iringa, basi la Majinja Express lilikuwa
likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam liligongana na lori na kisha
likaangukiwa na kontena lililosababisha vifo vya watu 43.
Mpekuzi blog
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
No comments:
Post a Comment