Monday, April 27, 2015
Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamebomoa kaburi la Napegwa Kishaluli (75) mkazi wa Mailimoja Kibaha mkoani Pwani aliyezikwa Aprili 20 mwaka huu na kumvua nguo zote pamoja na kuchukua mikoba aliyokuwa amezikwa nayo.
Tukio hilo lilitokea Aprili 24 mwaka huu katika Kata ya Tangini
jirani na soko la Loliondo ambako baada ya mazishi kaburi hilo
liliwekewa mlinzi kwa muda wa wiki moja.
Mkataba wa mlinzi huyo ulipomalizika aliondoka na siku iliyofuata kaburi hilo lilivunjwa.
Watu wa karibu na familia ya marehemu wamesema kuwa
baada ya mazishi ulikuwapo uvumi kwamba marehemu alizikwa na vitu vya
thamani zikiwamo fedha, simu, pete na mikufu ya dhahabu pamoja na nguo
zenye thamani kubwa.
Hata hivyo, taarifa zinasema marehemu Kishaluli alizikwa na mikoba
miwili ya nguo na vitu vyake vingine na kwamba kabla ya kifo chake
aliagiza azikwe na vitu vyake.
Akizungumza na Mwandishi wetu jana,ndugu wa marehemu,Bartholomew Mwanjile
alisema baada kuzika walilazimika kuajiri mtu wa kulinda kaburi hilo la
ndugu yao kwa wiki moja lakini siku moja baada ya mkataba kumalizika
kaburi hilo lilivunjwa.
“Tuliweka mlinzi alinde kaburi hilo kwa wiki moja tukiamini litakuwa limekauka kwa sababu lilitengenezwa kwa zege.
“Tuliamini watu wenye nia mbaya watashindwa kulivunja jambo ambalo
limekuwa kinyume kwa vile baada ya muda huo kumalizika kaburi
lilibomolewa na watu wasiojulikana ambao waliamini ndani ya mikoba hiyo
kulikuwa na fedha,” alisema Mwanjile.
Mwanjile alisema baada ya kuvunja kaburi hilo majambazi walifungua
jeneza na kupekua ndani kwa kuligeuza na kuliweka tofauti na lilivyokuwa
awali, baada ya kumvua marehemu nguo zote na viatu alivyokua
amevalishwa na hata soksi nazo walichukua.
Alisema tukio la kuvunjwa kwa kaburi hilo limetokea baada ya uvumi
kuwa ndugu yao alizikwa na nguo na vitu vingine zikiwamo fedha, kiasi
cha Sh milioni 8, cheni ya dhahabu,simu za gharama na kompyuta
mpakato(laptop),jambo ambalo si la kweli.
“Tulimzika ndugu yetu na mikoba ya nguo zake ambazo aliagiza kabla ya
mauti kumkuta na kaburi tulijenga kwa zege lakini tukashauriana tuweke
mlinzi, hapo ndipo watu wakaanza kutia shaka wakadhani kuna vitu vya
gharama jambo ambalo si kweli,” alisema Mwanjile.
No comments:
Post a Comment