Friday, April 17, 2015
Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, kimeitahadharisha serikali juu ya mpango wowote wa kutaka kuongeza muda kwa serikali yaawamu ya nne kuwepo madarakani, kwa kisingizio cha kutokamilika kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambao unafanyika kwa mfumo wa BVR.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa viongozi wa chama hicho wanaounda timu za kampeni za uchaguzi mkuu; Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amesema sintofahamu inayoendelea katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge, inalenga kuzuia uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi mkuu na hivyo kumpa Rais Kikwete muda zaidi wa kubaki madarakani.
Kwa mujibu wa Mbowe, uboreshaji wa daftari hilo unaweza usikamilike ndani ya kipindi cha miezi minne iliyobaki kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu na kuonya kuwa CHADEMA na UKAWA kwa ujumla hawatakubali kuona katiba ikivurugwa kutokana na ukaidi wa kufanya marekebisho madogo kwenye katiba iliyopo kama ilivyokubaliwa katika kikao cha pamoja cha vyama vinavyounda Kituo cha Kemokrasia - TCD.
Katika makubaliano hayo ya TCD ambayo chama cha CHADEMA ni mmoja wa wanachama, ilikubaliwa kuwa kufanyike marekebisho kwenye katiba ya sasa ambayo ni kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi itakayoaminiwa na wadau wote wa uchaguzi.
Marekebisho mengine ni kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi kwenye ngazi zote za uchaguzi mkuu sambamba na kusogeza mbele mchakato wa kutafuta katiba mpya mpaka baada ya uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa Mbowe hatua yoyote ya kutaka kuongeza muda wa serikali ya sasa kuwepo madarakani pamoja na kutokubali kufanyika kwa marekebisho hayo hapo juu kunaweza kuiingiza nchi katika matatizo makubwa ikiwemo machafuko.
No comments:
Post a Comment