Friday, April 17, 2015
MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu na viongozi wa dini ya Kiislamu nchini, wameungana kukemea vitendo vya uhalifu nchini.
Wamezitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto wao ili kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza katika vitendo hivyo.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na IGP Mangu na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu katika mwendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi hao katika kuimarisha usalama nchini.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na IGP Mangu na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu katika mwendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi hao katika kuimarisha usalama nchini.
Kaulimbiu
ya mafunzo hayo ilikuwa “Amani na usalama ndio maisha yetu”. Mafunzo
hayo yaliratibiwa na Taasisi ya Mwinyi Baraka na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa dini ya Kiislamu hapa nchini.
Mangu
alisema viongozi wa dini wana dhamana kubwa katika kuhakikisha vitendo
vya uhalifu, vinadhibitiwa nchini kwa kuwaelimisha waumini wao na jamii
kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu na kuwapa mafundisho yatakayojenga
na kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
Alisema
wahalifu wa sasa wana mbinu nyingi, hivyo kitu kikubwa kitakachoweza
kusaidia katika mapambano hayo ni mshikamano wa dhati kutoka kwa
viongozi hao katika kuwafichua ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mwakilishi
wa Shehe Mkuu wa Tanzania katika kikao hicho ambaye ni Mjumbe wa Baraza
Kuu la Ulamaa katika Baraza Kuu la Waislamu Nchini (BAKWATA), Shehe
Abubakar Zuberi alisema kuna haja ya kuziba nyufa za uvunjifu wa amani,
ambazo zimeanza kujitokeza hapa nchini.
Alisema
ni muhimu kuziba nyufa hizo kwa kuanzia kwenye misikiti, familia zao na
hatimaye katika jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha kuwa nchi
inaendelea kubaki salama kwakuwa amani tuliyonayo ni neema ambayo
tunapaswa kuilinda kwa nguvu kubwa.
“Vilevile
hatuna budi kuimarisha malezi katika familia zetu maana tunaposhindwa
kuwalea watoto wetu vizuri ndio chimbuko la kushamiri kwa vitendo vya
uhalifu wa aina mbalimbali hivyo tujielekeze katika kutoa mafunzo bora
katika familia,” alisema Shehe Zuberi.
Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, Shehe Khamis Mataka alisema
uhalifu unaweza kujitokeza sehemu yoyote na hata ndani ya msikiti hivyo
ni jukumu la viongozi wa misikiti kuwafichua wahalifu walio ndani ya
misikiti.
Akizungumzia
mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwinyi Baraka, Shehe Issa Othman
alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo viongozi wa
dini waweze kuwaelimisha waumini wao juu ya kukabiliana na vitendo vya
uhalifu ili kuimarisha ulinzi na usalama.
No comments:
Post a Comment