Hatimaye Rais Jakaya Kikwete amemtaja mrithi wake baada ya kuwataka wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kumchagua mgombea urais anayekubalika ndani na nje ya chama hicho.
Kikwete
alisema hayo jana wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu kwenye
ukumbi wa ofisi ya makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma, unaojulikana
kwa jina la White House.
Kauli hiyo imekuja wakati
chama hicho kikiwa kwenye wakati mgumu kupata mgombea mpya baada ya Rais
Kikwete kumaliza muda wake wa vipindi viwili vinavyokubalika kikatiba,
huku kukiwa na ongezeko kubwa la nguvu ya upinzani.
Juzi,
Kamati Kuu ya CCM iliwaachia huru makada wake sita waliotumikia adhabu
ya miezi 17 ya kuzuiwa kujishughulisha na shughuli za uchaguzi baada ya
kubainika kukiuka sheria za uchaguzi za chama hicho kutokana na kuanza
kampeni mapema.
Miongoni mwa makada hao, wamo wanaopewa
nafasi kubwa ya kupitishwa na chama hicho na ambao kambi zao zimekuwa
zikipambana vikali na kuweka wasiwasi wa kuivuruga CCM.
Lakini
Kikwete, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, alionekana kufahamu hali
inayoendelea na alitumia muda huo kueleza jinsi ambavyo CCM imejidhatiti
kupata mgombea urais kwa kuzingatia maslahi ya chama hicho na ya
Watanzania, akisema wakati wa kudhani mtu yeyote anayeteuliwa na chama
hicho atachaguliwa na wananchi umeshapita.
Akizungumza
kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Rais Kikwete alisema kikao cha
Halmashauri Kuu kina umuhimu wake kwa sababu kitaamua ushiriki wa CCM
katika Uchaguzi Mkuu na kutoa ratiba ya uteuzi wa wagombea wa chama
hicho.
Rais Kikwete alisema watu wote wanachama na wasio wanacha wanasubiri kwa hamu uamuzi wa vikao vya juu vya CCM.
“Watanzania
wote bila kujali itikadi zao wanaitazamia na kuitumainia CCM kutoa
uongozi ulio bora kwa nchi yetu. Hali hii inathibitisha ule usemi wa Baba
wa Taifa kwamba Rais anaweza kutoka chama chochote lakini rais bora
atatoka CCM,” alisema.
Alisema CCM inatakiwa kutambua
na kuzingatia uzito wa wosia huo wBaba wa Taifa na kuhakikisha kuwa
unatekelezwa kwa ukamilifu wake.
“Asiyesikia la mkuu
huvunjika guu. Vikao vya Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano
Mkuu wa Taifa, vina jukumu maalumu la kuongoza na kusimamia mchakato wa
uteuzi ndani ya chama, utakaotuwezesha kupata wagombea wanaofaa,”alisema.
“Wenye
kukidhi kiu na matarajio ya wanachama wa CCM na wananchi wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania ni sisi. Lazima tupate wagombea wanaochagulika,
tunapowapeleka kwa wananchi ambao wengi wao siyo wanaCCM.”
Alisema CCM wako milioni sita lakini wapigakura ni milioni 23, kwa hiyo lazima wapate mtu ambaye wananchi watamkubali.
Rais
Kikwete alisema wakimpata mtu ambaye wao CCM inampenda, lakini wananchi
hawatampenda, chama hicho kitaumia.
“Lazima tupate wagombea ambao wananchi watasema ‘naam’, tusipate wagombea ambao watu wataguna. Watasema ‘eeh yaani CCM wamemleta huyu? Tutauweka ushindi kwa CCM rehani. Ndugu zangu lazima tutambue kuwa wakati umebadilika,”alisema.
“Lazima tupate wagombea ambao wananchi watasema ‘naam’, tusipate wagombea ambao watu wataguna. Watasema ‘eeh yaani CCM wamemleta huyu? Tutauweka ushindi kwa CCM rehani. Ndugu zangu lazima tutambue kuwa wakati umebadilika,”alisema.
“Ni
ngumu sana kwenye chama chetu ukiwaambia kuwa wakati umebadilika na
tunaweza kushindwa, wanakuwa wagumu sana, lakini mnajidanganya tu,
lazima tujue kwamba wakati umebadilika... ile dhana kuwa yeyote
atakayeteuliwa na CCM atashinda imeshapitwa na wakati.”
Rais Kikwete alisema dhana ya kuwa wakichagua mtu yoyete mradi katoka CCM, watakuja kukiona cha mtema kuni.
“Hivyo
ni lazima tupate wagombea wanaochagulika na wananchi ambao niwengi
kuliko wanaCCM. Hatuwezi kupeleka kwa wananchi watu wasiokubalika, watu
waliopungukiwa sifa, tukadhani Watanzania watamchagua tu kwa sababu ni
mgombea wa CCM,” alisema.
“Lazima tuwe na wagombea
watakaopendeza kwetu na watakaopendeza kwa Watanzania. Wagombea ambao watu
wataamini kuwa wako salama, nchi,jimbo, kata zipo katika mikono
isiyokuwa na shaka.”
Alisema wakipeleka wagombea wanaowapendeza wao bila kuwapendeza wananchi, watakula hasara.
“Tutajipa
kazi kubwa ya kufanya na kuna hatari ya kushindwa. Lazima tusome alama
za nyakati. Tutambue zaidi watu wanachukizwa na watu wa namna gani?
"Tusipeleke mtu anayeakisi mambo yanayochukiza watu na kujiaminisha kwa historia na nguvu ya Chama cha Mapinduzi atashinda hampiti nimesema wakati ule ndugu zangu umekwisha,”alisema.
"Tusipeleke mtu anayeakisi mambo yanayochukiza watu na kujiaminisha kwa historia na nguvu ya Chama cha Mapinduzi atashinda hampiti nimesema wakati ule ndugu zangu umekwisha,”alisema.
“Tusidanganyane
kwamba sisi tunapendana au tunaogopana, wananchi hawatatuogopa.
Wananchi hawatakuogopa wala hawatasita kuonyesha kwamba hawapendezwi
naye.
"Tukifanya uteuzi mbaya wa wabeba bendera kwa urais, wabunge wawakishi madiwani hasira za wananchi zinaweza kuwa kwa chama kizima na kuadhibu wagombea wetu ngazi nyingine.”
"Tukifanya uteuzi mbaya wa wabeba bendera kwa urais, wabunge wawakishi madiwani hasira za wananchi zinaweza kuwa kwa chama kizima na kuadhibu wagombea wetu ngazi nyingine.”
Alisema wakipata mgombea ambaye wananchi wataguna, wananchi wanaweza wakapata hasira na wakawakataa wagombea wote.
Rais
Kikwete alitoa mfano wa chama cha nchini Canada ambacho kilikuw
kikiongoza tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, lakini kilipoenda katika
uchaguzi kikashindwa hata kuwa chama kinachoongoza katika upinzani ndani
ya Bunge.
“Ndiyo maana nasema sisi tusilewe historia kwamba chama kikubwa.
"Tukifanya makosa hatutafika. Tusikubali kukifikisha chama chetu hapo kwa sababu ya urafiki. Chama kwanza, mtu baadaye,” alisema.
Alisema
bahati nzuri CCM ina misingi mizuri ya kupata wagombea wake,labda
waamue wenyewe kutoiheshimu misingi hiyo ambayo imejengwa katika kanuni na
taratibu za kuwapata wagombea.
Rais Kikwete alisema
CCM ina maadili na miiko yake ya kuzingatia taratibu na kwamba miiko
hiyo imejaribiwa na kutumika na kuwapata wagombea wazuri waliokiletea
chama ushindi na heshima katika chaguzi zilizopita.
“Nawaahidi
hatutayumba wala hatutaogopa katika kusimamia misingi hii mizuri ya
chama chetu, kwa nia ya kukumbushana dhima na wajibu wa wanachama na
viongozi tulio nao katika kulitekeleza hili,” alisema.
Aliwataka kuongozwa na kuweka masilahi mapana ya chama chao, kuliko masilahi ya mtu mmoja mmoja.
“Nayasema
haya kwa sababu naona kumekuwepo kujisahau au kujifanya kuwa umesahau
miongoni mwa wagombea wa uteuzi na hata miongoni mwa wajumbe wa
Halmashauri Kuu na viongozi wengine wa chama na hata wanachama kwa kufanya
mambo mengine yaliyo kinyume na misingi ya chama,” alisema.
“Tusitoe
nafasi ya kukimong’onyoa chama, haiwezekani yanaposema ama inaposikika
minong’ono baina ya wagombea, washabiki na baadhi yetu tukiwemo humu
(Nec), hayanifurahishi hata kidogo.”
Alisema watu kufanya mambo yaliyo kinyume na uteuzi ndani ya chama mambo yasiyokubalika, hayataachwa yapite.
“Naomba
myazingatie ili mrahisishe kazi ya uteuzi, tujadili tu historia ya mtu
na uwezo wake kwa nafasi anayoiomba. Isiwe tunapoteza muda mwingi
kujadili makando kando, mambo yanayofanyika kinyume cha utaratibu.
Utafanyaje mambo kinyume cha utaratibu unataka kukipeleka wapi chama
chetu?
“Mnataka iweje, tuseme hakuna kilichofanyika? Haiwezekani hatuwezi kunyamaza
tutakuwa tumepoteza dhamana yetu. Tunao wajibu wa kusimamia misingi
tuliojiwekea na kikao hiki ndicho chenye dhamana hiyo"alisema.
Alisema
wamedhamiria kusimamia bila ajizi, bila kupendelea na kwamba wana wajibu
wa kutenda haki na watafanya hivyo na bila shinikizo kutoka kwa mtu
yoyote.
“Bila shaka viongozi wenzangu tumeelewana, tusaidiane ili tuvuke vyema,” alisema.
Alisema Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 bado inaandaliwa na imefikia mahali pazuri na kwamba kikao kijacho itapelekwa.
Katika
hatua nyingine, Kamati Kuu ya CCM imeishauri Serikali kukutana na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Nec, kutafakari namna bora ya kushughulikia kura
ya maoni kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari
jana kuwa CCM imeangalia changamoto zilizopo na hivyo kutoa ushauri
huo.
“Moja ya changamoto ni suala la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Wapigakura,” alisema.
Kamati Kuu jana mchana ilimaliza kikao chake kilichofanyika kwa siku mbili.
Kamati hiyo ilikutana tangu juzi saa 10:00 jioni na kuendelea hadi saa nane za usiku wa kuamkia jana.
Hata
hivyo, taarifa zinaeleza kuwa kamati hiyo ilikuwa bado haijamaliza
baadhi ya ajenda na hivyo kukutana tena jana saa sita mchana hadi
walipomaliza alasiri na ndipo Halmashauri Kuu ya Taifa ilianza kikao
chake saa 10 alasiri badala ya saa nne asubuhi.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka ndani ya CC, zilidai kulikuwa na mvutano kuhusu
ratiba ya mchakato wa kutafuta wagombea wa nafasi za urais, ubunge,
udiwani na uwakilishi kutokana na muda kuonekana kuwatupa mkono na
kanuni.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya CC, kilidai kuwa suala la ratiba lilikuwa na mvutano kwakuwa muda umekwenda.
Kwa
mujibu wa utaratibu, wanaoomba nafasi ya kuteuliwa kugombea urais,
lazima wapate muda wa kutafuta wadhamini katika mikoa mbalimbali ya Bara
na Visiwani.
Wagombea hao baada ya kupata wadhamini
wanatakiwa kupita kwenye mchujo wa vikao vya chama, kuanzia Kamati Kuu,
Halmashauri Kuu ya Taifa na baadaye Mkutano Mkuu.
Baada
ya kupatikana mgombea urais, jina lake linatakiwa kupelekwa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, Nec, ambako nako hutolewa muda kwa wanaotaka kuweka
pingamizi.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa CC pia ilikuwa na
changamoto kuhusu kanuni, na kuna taarifa baadhi ya wabunge wanataka
kanuni zimtambue mbunge kuwa ni mjumbe halali wa Halmashauri Kuu.
Hali ilivyokuwa
Jana
asubuhi kabla ya kikao cha CC, kilianza kikao cha Kamati Maalumu ya
Zanzibar ambao walikuwa wakipitisha majina ya wagombea katika nafasi za
uongozi wa chama kupitia Shirikisho la Vyuo Vikuu.
Wajumbe wa Nec waliambiwa kikao kingeanza saa nne, lakini baadaye
zikasambaa taarifa kwamba CC ilikuwa haijamaliza baadhi ya ajenda,
wajumbe wakalazimika kuendelea kusubiri, lakini baadaye walipewa
makablasha kwa ajili ya kujiandaa na kikao chao kilichoanza saa 11
jioni.
Hata hivyo, mmoja wa wanaotafuta kuteuliwa kuwa
wagombea urais alionekana akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Nec
akiwathibitishia yuko ‘serous’.
Mmoja wa wajumbe wa Nec alithibisha kwamba alifuatwa na mgombea huyo akiomba aungwe mkono.
Pia baadhi ya mashabiki wa watangaza nia walikuwepo wakiwa kwenye makundi yaliyoashiria ni kupanga mikakati ya kukubalika.
Noti zamwagwa
Taarifa
zingine zilidai kuwa juzi watangaza nia wawili walio kwenye nafasi za
uwaziri, walianza kumwaga fedha kwa wajumbe wa Nec, mmoja anaelezwa kutoa
‘mshiko’ wa Sh300,000 kwa kila mjumbe na mwingine alimwaga ‘mshiko’ wa
Sh500,000 kwa wajumbe.
Baadhi ya wajumbe ambao hawakupata ‘mshiko’ huo waliliambia Mwananchi kwamba, wamesikia wenzao wamepewa lakini wao hawakupewa.
Baa zafurika
Baada
ya taarifa za kufutwa kwa kifungo kwa makada sita, waliofungiwa kwa
kukiuka kanuni za kuanza kampeni mapema, baa nyingi katika mji wa
Dodoma, zilifurika baadhi ya wapambe wa watangaza nia, ambapo walikunywa
na kula wakishangilia uamuzi wa CC wa kuwafungulia makada hao.
Hata
hivyo, hali hiyo ilikuwa tofauti na upande wa watangaza nia waliotaka
mmoja wao akatwe, ambapo mmoja wa wapambe hao ambaye ni mbunge (jina
linahifadhiwa) alisikika akimweleza mwenzake kuwa “mjomba tumekufa”.
Zanzibar watoa neno
Vyama
vya Upinzani Zanzibar vimepongeza hatua ya CC ya kuwaachia huru makada
wake sita ambao walifungiwa kushiriki harakati za kisiasa baada ya
kwenda kinyume na maadili ya kuanza kampeni mapema kabla ya utaratibu wa
chama kutangazwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
Viongozi wa TADEA, CHADEMA, CUF, CCM, ADC walisema kitendo cha CCM
kuwachukulia hatua makada wake sita, ambao ni viongozi mashuhuri ni
mfano tosha kuwa chama hicho hakijali mkubwa wala tajiri katika
kusimamia miiko na maadili ya chama.
“Sisi kama TADEA
tunawapongeza CCM kwa kusimamia taratibu na misingi ya demokrasia na hii
ni fundisho kwa vyama vyengine kuheshimu miiko na maadili ya chama”
alisema Juma Ali Khatib, Katibu Mkuu wa Tadea.
Hata
hivyo, alisema kwamba katika kipindi kama hiki cha kuelekea kwenye
uchaguzi pilikapilika pamoja na harakati za nje ya mfumo wa chama
haziwezi kukwepeka kwa sababu hakuna wapambe wanaoweza kukaa kimya bila
ya kumfanyia kampeni mgombea wao.
Kwa upande wake Naibu
Katibu mkuu wa ADC, Ali Makame Issa alisema kwamba kuna mambo ya
kujifundisha kutoka CCM kama chama ambacho hakijali cheo cha mtu, sifa
au uwezo wake, na kusimamia maadili kwa vitendo tofauti na vyama
vyengine.
Alisema CCM kama chama tawala lazima
kiangalie kitarudisha vipi umoja baada ya kupata jina moja la mgombea
wake wa nafasi ya Urais, na kusisitiza upo umuhimu wa kuzingatia haki na
usawa na kuondoa mizengwe katika kupata jina la mgombea wa chama hicho.
Katibu
wa Umoja wa Vijana wa Chadema Mkoa wa Mjini Magharibi (BAVICHA) Francis
Werema alisema CCM imejitisha yenyewe ndio maana imeamua kuwafungulia
makada wake baada ya kuona hawana mtu mwenye sifa ya kuwania Urais zaidi
ya watu sita waliokuwa wamefungiwa.
“Wamehofia
kuathiri uhai na umoja wa chama chao katika kuelekea uchaguzi mkuu,
baada ya kuona wamejitokeza wagombea wengi , wengine wakikosa sifa za
kushika nafasi hiyo ikilinganishwa na makada sita waliofungiwa” alisema
Werema.
Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Omar
Ali Shehe alisema uamuzi wa kuwafungulia makada sita ni mbinu ya
kuwaziba macho watu, kwa vile huwezi kumfungia mtu kwa makosa
yaliyothibitika na baadae kupata msamaha.
Alisema
kwamba chama chochote kinahitaji kusimamia kwa vitendo harakati na
shughuli zake za kisiasa kwa kuzingatia miiko na maadili na ndio maana
CUF imeagiza kitengo cha ulinzi cha chama hicho kuanza kufuatilia na
kuchunguza wabunge na wawakilishi ambao wanatuhumiwa kutumia ushawishi
wa rushwa wakati wa zoezi la kura za maoni.
Naye Katibu
Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mjini, Baraka Shamte alisema kwamba adhabu
iliyokuwa imetolewa na chama imeweka msingi wa nidhamu kwa viongozi
lakini alisema wakati umefika miiko na maadili ya chama yasimamiwe
kuanzia ngazi ya tawi, wilaya hadi mkoa, kwa sababu kuna viongozi
wanaokiuka miiko na maadili ikiwemo Zanzibar.
“Hata
majambazi wana maadili yao, wanalishana hadi yamini yakutokutoa siri, na
wapo tayari kufa napongeza sana hatua iliyochukuliwa ya kuwasamehe,”
alisema Baraka Shamte.
Shangwe za wanachama wa CCM
zilianza kujitokeza katika maskani mbalimbali zanzibar, muda mfupi
baada ya kutolewa kwa taarifa za kusamehewa kwa makada sita waliokuwa
wamefungiwa kujulikana huku Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa akipewa
nafasi kubwa katika mazungumzoa ya wana maskani ikiwemo maskani Kaka ya
Kisonge, Naushad Maskani Jang’ombe, Dk.Omar maskani, pamoja na baraza
mbalimbali za wanachama wa kambi ya upinzani pia walionekana kufuatilia
taarifa hizo kupitia vituo vya radio na televisheni zanzibar.
No comments:
Post a Comment