Sunday, May 24, 2015

Wanandoa Wauawa Kwa Kuchinjwa Kama Kuku


Watu wawili, mke na mume wakazi wa  Makambo, wilayani Mlele, wameuawa kikatili kwa kuchinjwa na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili wakati wakiwa wamelala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, aliwataja wanandoa hao  kuwa ni  Seth Mwakalimbwa (65) na Yakoba  Kalulu (48).
 
Kidavashari aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Mei 21, usiku nyumbani kwa wanandoa hao ambao baada ya kuuawa miili yao iliachwa kitandani.

Alisema marehemu hao wakati wa uhai wao walikuwa wakiishi kwenye nyumba yao peke yao kwa muda mrefu.

Alisema,  balozi wa eneo hilo, Wilbroad Mahenge, ndiye aliyegundua vifo hivyo baada ya kutowaona wanandoa hao kwa siku mbili mfululizo na kuingiwa na wasiwasi.

Kamanda Kidavashari alisema balozi huyo aliamua kwenda kwenye nyumba ya wanandoa hao ili kujua hali zao na alipofika alikuta  milango ikiwa wazi hali iliyosababisha apate mashaka.

Alisema alijaribu kuwaita kwa majina yao lakini hakuna aliyeitika na aliamua kuingia ndani na kuwakuta wakiwa wamelazwa kitandani huku wakiwa wamefariki dunia kwa kuchinjwa shingo zao na kutenganishwa kiwiliwili na kichwa.

Alisema, balozi Wilbroad alikwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa serikali ya kitongoji ambao nao walitoa taarifa polisi.

Kamanda alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.
 
Aidha, alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Alisema polisi kwa kushirikiana na uongozi na wanakijiji wa Makambo, wanaendelea na msako ili kuwabaini watu waliohusika katika mauaji hayo

No comments:

Post a Comment