MATOKEO YA UCHUNGUZI WA AWALI KUMHUSU NDUGU ELIAKIM C. MASWI, KATIBU MKUU, WIZARA YA NISHATI NA MADINI
_________________________________________________
1.0 Utangulizi
1.1
Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, pamoja na mambo mengine, lilijadili Taarifa ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyotokana na Taarifa ya Ukaguzi
wa Akaunti ya Tegeta Escrow uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali.
1.2 Baada ya majadiliano, Bunge lilipitisha maazimio kadhaa yaliyoelekezwa kwa Serikali kwa ushauri na utekelezaji.
Mojawapo
ya maazimio hayo yalimtaja Ndugu Eliakim C. Maswi, ambaye ndiye Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kuwa amehusika kijinai au kimaadili
katika miamala iliyotokea katika akaunti ya Tegeta Escrow.
1.3
Wakati anahutubia Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam tarehe 22
Desemba, 2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema
ifuatavyo:-
“Kuhusu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa
Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma. Hivyo,
nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana
makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
1.4
Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi zimeshughulikiwa katika ngazi
mbili tofauti. Amechunguzwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma, kisha
baada ya hapo alichunguzwa pia na Kamati ya Uchunguzi wa Awali
iliyoundwa na mamlaka yake ya nidhamu.
2.0 Sekretarieti ya Tume ya Maadili
2.1
Kifungu 18 (2) (c) na (3) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
kinaipa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mamlaka na uwezo wa
kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa maadili ya uongozi wa umma
yanayotawaliwa na Sheria hiyo.
Tuhuma dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi zilizomo kwenye maazimio ya Bunge zinatawaliwa na Sheria hiyo.
2.2
Katika kutekeleza majukumu yake, Sekretarieti ya Maadili ya Umma
ilifanya uchunguzi wa awali na kisha kumhoji Ndugu Eliakim C. Maswi
tarehe 19 Desemba, 2014.
2.3
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haijabaini kuwepo kwa
maslahi binafsi katika uamuzi uliofanywa na Katibu Mkuu, Wizara ya
Nishati na Madini wa kuruhusu fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow
kutolewa.
Aidha, hawakubaini ukiukwaji wowote wa maadili ya viongozi wa umma uliofanywa na Ndugu Eliakim C. Maswi.
Waliona
kuwa yote aliyoyafanya yalizingatia matakwa ya Sheria, ushauri wa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na ridhaa ya TANESCO. Hivyo,
Sekretarieti ya Maadili haikuona msingi wowote wa kuendelea na shauri la
Ndugu Eliakim C. Maswi, na wamelihitimisha.
3.0 Kamati ya Uchunguzi wa Awali ya Mamlaka ya Nidhamu
3.1
Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya
mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa) Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya
Nidhamu ya Makatibu Wakuu.
3.2
Kwa kuzingatia Azimio husika la Bunge, na kwa maelekezo ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi aliunda Kamati ya
Uchunguzi wa Awali dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, chini ya Kifungu cha 36 cha Kanuni za
Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kinachotamka ifuatavyo:-
“Where
it is necessary to institute disciplinary proceedings against a public
servant, the disciplinary authority shall make preliminary
investigations before instituting disciplinary proceedings.”
3.3
Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni 35(2)(b) na Kanuni 37 ya Kanuni
za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Katibu Mkuu Kiongozi alimpumzisha
Bwana Eliakim C. MASWI kutekeleza majukumu yake ya kazi ya Katibu Mkuu
ili kupisha uchunguzi wa awali.
Uchunguzi
wa awali ulifanyika chini ya Kanuni ya 36 ya Kanuni za Utumishi wa Umma
zilizotajwa, pamoja na Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma
Na. 8 ya mwaka 2002, kama ilivyorekebishwa.
3.4
Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kanuni zilizotajwa kwenye ibara 3.3 hapo
juu, Katibu Mkuu Kiongozi aliteua Kamati ya Uchunguzi wa Awali na kuipa
Hadidu za Rejea zifuatazo:
3.4.1
Kubainisha wajibu na madaraka halisi ya Katibu Mkuu, Wizaraya Nishati
na Madini, kwenye uendeshaji wa TANESCO kwa ujumla, na hususan kwenye
kufungua, kuendesha na hatimaye kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow.
3.4.2 Kubainisha
na kupata maelezo ya kina juu ya kuhusika kwa Bwana Eliakim C. Maswi
katika mchakato na mtiririko mzima wa akaunti ya Tegeta Escrow, tangu
kufunguliwa hadi kufungwa.
3.4.3
Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo kuna jambo lolote ambalo
Bwana Eliakim C. Maswi alilifanya au ambalo alipaswa kulifanya lakini
hakulifanya, linalomstahilisha achukuliwe hatua za nidhamu.
3.4.4
Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo katika hatua yoyote ya
mchakato na mtiririko wa tangu kufunguliwa hadi kufungwa kwa akaunti ya
Tegeta Escrow, Bwana Eliakim C. Maswi alifanya jambo lolote
linalodhihirisha matumizi mabaya ya mamlaka yake kama Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, kwa namna iliyosababisha hasara ya aina
yoyote ile kwa Taifa la Tanzania.
3.4.5
Kubainisha na kupata maelezo ya kina iwapo katika hatua yoyote tangu
akaunti ya Tegeta Escrow ilipofunguliwa hadi ilipofungwa, Bwana Eliakim
C. Maswi hakuchukua tahadhari ya kutosha kulinda maslahi ya umma na
kusababisha kupotea kwa fedha za umma kwa uzembe au matumizi mabaya ya
madaraka.
3.4.6
Kubainisha iwapo kuna mahali popote katika mchakato wa akaunti ya
Tegeta Escrow ambapo Bwana Eliakim Chacha Maswi alifanya jambo lolote
linaloashiria kitendo cha kijinai, au kukiuka maadili ya viongozi wa
umma.
3.4.7
Kuandaa taarifa ya uchunguzi wa awali kwa msingi wa Hadidu za Rejea
zilizomo humu na kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Taarifa hiyo,
pamoja na mambo mengine, ipendekeze hatua za kuchukuliwa kwa kila eneo
ambalo Kamati itabaini umuhimu wa hatua kuchukuliwa.
3.5 Mapendekezo ya Kamati ya Uchunguzi wa Awali
3.5.5
Kamati haijabaini kosa lolote ambalo linaweza kusababisha Ndugu Eliakim
Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, kufunguliwa
mashtaka ya kinidhamu kwa kukiuka Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298
ikisomwa pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 kwa kuruhusu Benki Kuu ya
Tanzania kutoa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
4 Hitimisho la Uchunguzi wa Awali
4.4
Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Sekretarieti ya Maadili umebaini kuwa
Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote ya kimaadili katika mchakato
wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
4.5
Hali Kadhalika Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Kamati ya Uchunguzi wa
Awali iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi umebaini kuwa Ndugu Eliakim C.
Maswi, “hakutenda au kuhusika na jambo lolote linaloashiria vitendo vya
jinai au kukiuka Maadili ya Viongozi wa Umma”.
4.6
Ushahidi wa vielelezo uliotolewa kwenye Sekretarieti ya Maadili na
kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Awali umejitosheleza kuthibitisha kwamba
Ndugu Eliakim C. Maswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha
kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali na kwa nyakati tofauti kwa
lengo la kuhakikisha na kujiridhisha kwamba kufungwa kwa Akaunti ya
Tegeta Escrow kunafanyika kwa usahihi.
4.7
Hakuna ushahidi wowote kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi alikuwa miongoni mwa
waliopata mgao wa fedha au fadhila yoyote kutokana na kufungwa Akaunti
ya Tegeta Escrow.
4.8
Kwa nafasi yake ya mamlaka ya nidhamu Katibu Mkuu Kiongozi, ameridhika
kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote aliyoyafanya katika
mchakato wa akaunti ya Tegeta Escrow yanayostahili adhabu.
No comments:
Post a Comment