Friday, May 8, 2015

SAKATA LA OPARESHENI TOKOMEZA: Ikulu Yasema Mawaziri WOTE Waliofukuzwa Kwa Kashfa Hiyo Hawana HATIA

Friday, May 8, 2015


TAARIFA YA KUKAMILIKA KWA KAZI YA TUME YA UCHUNGUZI WA MALALAMIKO YALIYOTOKANA NA UTEKELEZAJI WA OPERESHENI TOKOMEZA
1.0    Utangulizi:

1.1 Tarehe 01/05/2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliunda Tume ya Uchunguzi kuhusu malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Aliteua Makamishna watatu ambao ni Mhe. 
 
Balozi Jaji (Mst) Hamisi Amiri Msumi (Mwenyekiti wa Tume), Mhe. Jaji (Mst) Stephen Ernest Ntashima Ihema (Kamishna), Mhe. Jaji (Mst) Vincent Kitubio Damian Lyimo (Kamishna) na Ndugu Frederick Kapela Manyanda (Katibu wa Tume).

1.2  Operesheni Tokomeza ilikuwa Operesheni iliyobuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo jema na muhimu la kupambana na ujangili unaotishia urithi wetu wa wanyama pori, hususani tembo, faru, nyati, twiga, pundamilia n.k.

2.0  Hadidu Rejea kwa Tume

2.1Kuchunguza namna Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa;

2.2.Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;

2.3.Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;

2.4.Kuchunguza iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na maafisa wa Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao zilikuwa sahihi;

2.5.Kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya maaafisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea za Operesheni Tokomeza; na

2.6.Kupendekeza mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika kupanga na kutekeleza Operesheni nyingine kama hii ili kuzuia na kuepuka malalamiko mengine kama yaliyotokea kwenye Operesheni Tokomeza.

3.0    Kukamilika kwa kazi ya Tume

3.1  Tume imekamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe      10 Aprili, 2015. Kwa maagizo ya Rais tumeisoma na kuichambua taarifa hiyo vya kutosha. 
 
Kwa hakika Tume imefanya kazi kubwa sana, na nzuri sana ya uchunguzi na uandishi wa taarifa. Kazi imefanywa kwa weledi na umakini wa hali ya juu na kwa lengo dhahiri la kutenda haki. Katika siku 265, Tume ilitembelea wilaya 38 katika mikoa 20 na kuhoji jumla ya mashahidi 259. 
 
Mikoa iliyohusika ni Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani, Tabora, Singida, Manyara, Arusha na Tanga.

3.2 Tume imejitahidi kuwahoji wote waliokuwa na malalamiko, kuwahoji mashuhuda, kuwahoji watuhumiwa, na kukusanya ushahidi wa aina mbalimbali ili ama kuthibitisha makosa pale yalipofanyika na kupendekeza hatua za kuchukua, au kujiridhisha kuwa tuhuma na malalamiko hayakuwa ya msingi.
 
 Kazi hiyo imefanywa vizuri na kurahisisha kazi ya Serikali ya kuchukua hatua zinazostahili.

4.0    Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa 

4.1   Tume ilibaini kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja cha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza iliyoanza tarehe 4 Oktoba, 2013, mafanikio mengi yalipatikana, ikiwemo:

4.1.1 Watuhumiwa 1,030 wa makosa mbalimbali yanayohusu ujangili na uvunaji haramu wa misitu walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria;

4.1.2   Kukamatwa kwa meno ya 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya ngiri 11, mikia ya wanyama mbalimbali 36, ngozi za wanyama mbalimbali 21, pembe za swala 46, mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 waliokuwa wanachungwa ndani ya hifadhi na misitu, baiskeli 58, pikipiki 8 na magari 9;

4.1.3  Katika kipindi cha Operesheni kulikamatwa jumla ya bunduki za kijeshi 18, bunduki za kiraia 1,579, risasi 1,964, mbao vipande 27,913, mkaa magunia 1,242, magogo 858 na misumeno 60.

4.1.4  Operesheni ilifanikiwa kupunguza kasi ya mauaji ya tembo kutoka tembo wawili kwa siku hadi tembo wawili kwa mwezi wakati wa Operesheni;

4.2 Operesheni ilisitishwa rasmi tarehe 01/11/2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko yaliyojitokeza. Baada tu ya kusitishwa kwa Operesheni wafugaji wengi wamerudisha mifugo yao katika maeneo ya hifadhi yaani Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu na Maeneo Oevu na ujangili ukaanza kurejea. 
 
Aidha watuhumiwa waliokuwa wametoroka kukimbia Operesheni wameanza kurejea kwenye makazi yao.

5.0 Vitendo vya Ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea

5.1 Tume imebaini kuwa katika utekelezaji wa Operesheni kulikuwa na matukio ya ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea. Ukiukwaji huu umesababisha madhara kwa wananchi mbalimbali ikiwemo vifo, madhara ya mwili na kadhalika.

5.2  Tume ilichunguza matukio 15 ya vifo, na kuridhika kuwa vifo tisa (9) kati ya hivyo vilisababishwa na mateso ambapo watendaji kwenye Operesheni walitumia nguvu kubwa kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati wa ukamataji au kuhoji.
 Kabla ya vifo watu hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na kuna ushahidi wa kitabibu (medical reports), ushahidi wa kimazingira na ushahidi wa kuona, unaohusisha vifo vya marehemu hao na mateso kutoka kwa askari wa Operesheni. 
 
Tume haikupata ushahidi wa kuhusisha vifo sita (6) vilivyobaki moja kwa moja na Operesheni Tokomeza.

5.3 Tume ilichunguza madai ya mateso yaliyosababisha madhara kwenye miili ya wahusika. Walalamikaji walieleza Tume kwamba waliteswa ili waoneshe silaha au nyara zilipofichwa au wakiri kujihusisha na ujangili au ujambazi na wataje washirika wao wa mtandao wa ujangili. 
 
Kulikuwa pia na malalamiko ya udhalilishwaji. Malalamiko hayo yalitoka kwenye wilaya ishirini na mbili (22) za mikoa mbalimbali. 
 
Yapo matukio ambayo walalamikaji waliweza kuleta mbele ya Tume uthibitisho wa kuteswa, na walionesha makovu na kutoa vyeti vya matibabu na PF 3 walizopewa baada ya kuumia.

5.4 Tume imebaini kuwepo matendo mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea uliofanywa na baadhi ya askari wa Operesheni na maafisa wengine walioshiriki katika utekelezaji wake, ikiwemo matukio yanayoashiria rushwa na udanganyifu mbalimbali.

5.5 Tume ilishughulikia pia tuhuma za wizi, upotevu na uporaji wa mali. Walalamikaji wa kundi hili walieleza Tume kuwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni, waliibiwa au kupoteza fedha na mali zao wakati na baada ya kukamatwa au kupekuliwa na askari wa Operesheni. 
 
Tume ilichunguza jumla ya matukio ishirini na tatu (23) ya aina hiyo na kubaini kuwa malalamiko mengi yalitokana na askari wa Operesheni kutofuata sheria, kanuni na taratibu za ukamataji, kuhoji na upekuzi maungoni mwa watuhumiwa na kwenye nyumba zao.
 
Kasoro zilizoonekana ni pamoja na kutoshirikisha viongozi au watu huru katika upekuzi na kutojazwa hati za upekuzi mara baada ya upekuzi. Kasoro nyingine ni askari wengi kuingia kwenye nyumba kwa wakati mmoja. 
 
Aidha, Tume imebaini walalamikaji wengine waliongeza chumvi katika ushahidi wao kuhusu idadi ya mali na fedha zilizopotea au kuibiwa na hivyo ushahidi wao kutoaminika au kuthibitika.

5.6 Tume ilichunguza malalamiko ya kubakwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni. Matukio yaliyochunguzwa na Tume yalikuwa katika Kijiji cha Iputi, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro na Kijiji cha Mwantimba Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu na Wilayani Sikonge. 
 
Hata hivyo wote waliodai kubakwa hawakujitokeza mbele ya Tume kutoa ushahidi wao, hivyo Tume haikuweza kuchunguza malalamiko yao. 
 
Alijitokeza mlalamikaji mmoja Wilayani Ulanga, Morogoro, lakini Tume haikuridhika na maelezo yake, ambayo hayakutosheleza kubainisha kosa kwenye utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.

5.7 Tume ilibaini kuwa wapo watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kutiwa hatiani na wengine kuachiwa. Tume imeona kuwa hatua hii ilikuwa sahihi kisheria. Lakini Tume ilibaini pia kuwa baadhi ya watuhumiwa hawakufikishwa mahakamani. 
 
Badala yake maafisa wa Operesheni walijichukulia mamlaka ya kutoa adhabu kwa watuhumiwa kama vile kukamata na kuzuia mali zao, kuchoma moto nyumba na mali zilizokuwa kwenye maeneo ya hifadhi, kuua au kujeruhi mifugo iliyokutwa kwenye maeneo ya hifadhi au kuuza kwa mnada ng’ombe waliokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi. 
 
Hatua nyingine inayolalamikiwa ni kuchukua bunduki zinazomilikiwa kisheria.

5.8  Tume imebaini kwamba katika baadhi ya maeneo askari wa Operesheni walichoma nyumba moto kwa madai ya nyumba hizo kujengwa kwenye hifadhi. 
 
Malalamiko hayo yalitoka katika Wilaya za Mlele na Mpanda, Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya; Wilaya za Nkasi na Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa; na Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara. 
 
Katika uchunguzi wa matukio haya Tume imebaini yafuatayo:

  • Wanakijiji hawakupewa taarifa ya kutosha kuhamisha mali zao kabla ya kuchoma nyumba zao;
  • Baadhi ya wanakijiji walipoteza vyakula na mali zao katika zoezi hilo la uchomaji moto;
  • Kuna vijiji vilivyosajiliwa lakini sehemu ya vitongoji vyake viko ndani ya Hifadhi za Taifa;
  • Kuna maeneo ya hifadhi au ushoroba (buffer zone) ambayo hayana alama za mipaka kati ya hifadhi  au ushoroba na vijiji husika;
  • Kuna nyumba ambazo hazikuwa kwenye eneo la hifadhi au ushoroba na hivyo zilichomwa moto kinyume cha sheria. 
  • Baadhi ya matukio na malalamiko ya kuchomewa moto nyumba yalitokea kabla ya Operesheni.

5.9  Uchunguzi wa Tume umebaini kuwepo kwa tatizo kubwa la wafugaji kutoka nje ya nchi na wafugaji wenyeji kuingiza mifugo yao katika Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Misitu, Maeneo Oevu na Hifadhi za Taifa. 
 
Maeneo yaliyoathirika sana na tatizo hili ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba la Kigosi – Moyowosi, Pori la Akiba la Maswa, Mapori ya Akiba ya Biharamulo – Burigi – Kimisi na Pori la Akiba la Kijereshi.

Katika baadhi ya maeneo imethibitika kwamba wapo ng’ombe waliouawa kwa kupigwa risasi baada ya kukutwa ndani ya hifadhi.
   
Aidha, Tume imeridhika kwamba kuna ng’ombe wa walalamikaji waliokamatwa na kuuzwa kwa mnada. Uuzaji wa ng’ombe katika tukio hili haukuzingatia utaratibu wa kisheria.

5.10 Tume ilipata ushahidi kwamba katika maeneo mbalimbali askari wa Operesheni walikamata au kuchukua bunduki, risasi pamoja na vitabu vyake hata kwa silaha zinazomilikiwa kihalali. 
 
Maeneo ambayo yalikuwa na malalamiko ya watu kuchukuliwa silaha zao ni mikoa saba (7) ambayo ni Katavi, Mbeya, Lindi, Morogoro, Tabora, Manyara na Pwani ambapo jumla ya watu sitini na mbili (62) walijitokeza mbele ya Tume kulalamika tukio hili.

6.0  Hatua Zitakazochukuliwa na Serikali

6.1  Baada ya kupitia kwa kina taarifa ya Tume, pamoja na mapendekezo ya Tume, Serikali itafanya yafuatayo:

6.1.1  Hatua za kimashtaka zitaendelea kwa shauri la mauaji ambalo upelelezi wake umekamilika na hatua za kiuchunguzi zitaendelea kwa mashauri mengine nane (8) ya mauaji ambayo upelelezi wake haujakamilika;

6.1.2  Hatua za kisheria na kiutawala zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliothibitika kuwatesa watu 15 wakati wa Operesheni;

6.1.3 Hatua za kiuchunguzi zinazofanywa na TAKUKURU kuhusu tuhuma za rushwa na udanganyifu zilizothibitika zitaendelea;

6.1.4 Silaha zinazodaiwa kumilikiwa kihalali zitafanyiwa uhakiki na ukaguzi wa kina kuhusu umiliki na matumizi yake na endapo hakutakuwa na sababu nyingine za kisheria za kuzuia urejeshwaji, wamiliki warejeshewe silaha zao kwa mujibu wa sheria na taratibu;

6.1.5 Mali ambazo zimethibitika kuchukuliwa wakati wa Operesheni kwa tuhuma za kuhusishwa na uvunaji haramu wa mazao ya misitu zirejeshwe endapo hakutakuwa na sababu za kisheria kuendelea kuzishikilia;

6.1.6 Serikali itafanya uhakiki wa vijiji ambavyo vimesajiliwa na vimo ndani ya hifadhi ili kutatua migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na vijiji. Aidha, Serikali itahakikisha kunakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya Msajili wa vijiji au mamlaka husika  na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuepuka kusajili vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi;

6.1.7 Wizara ya Maliasili na Utalii itatayarisha kanuni zitakazoweka utaratibu wa kuwaondoa watu waliovamia na kujenga makazi katika hifadhi;

6.1.8 Sheria zote zinazolinda maeneo ya hifadhi zitafanyiwa marekebisho ili kuongeza adhabu kwa kosa la kuingiza mifugo kwenye Hifadhi bila kujali uraia wa wamiliki wa mifugo hiyo;

6.2 Kwa vile Tume imejiridhisha na faida kubwa na mafanikio ya Operesheni    Tokomeza, Serikali itaendelea na Operesheni kama hizo kadri     itakavyojitajika ili kuokoa maliasili za Taifa, ikiwemo wanyama, hifadhi     na misitu. 
 
Hata hivyo ushauri wa Tume juu ya kuboresha upangaji,     usimamizi na utekelezaji wa Operesheni hizo itazingatiwa kikamilifu.

7.0    Mawaziri Waliojiuzulu
Tume ilijiridhisha kuwa Mawaziri wote waliojiuzulu, yaani Mhe. Dkt. Emmanuel J. Nchimbi, Mb., Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb., Mhe. Mathayo D. Mathayo, Mb., na Mhe. Shamsi V. Nahodha, Mb., hawakuhusika moja kwa moja na makosa yoyote ya utekelezaji kwenye Operesheni Tokomeza. Hivyo, waliwajibika kisiasa tu na hakuna hatua nyingine inayostahili dhidi yao

No comments:

Post a Comment