Sunday, June 7, 2015

Kinana atahadharisha ujenzi soko la ghorofa


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amehadharisha Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba dhidi ya mpango wake wa kujenga soko la ghorofa kwa kuitaka ijifunze kilichoikumba Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kujenga soko la Machinga Complex .

Hadhari hiyo aliitoa juzi katika mkutano wa hadhara katika eneo la Kashai, mjini Bukoba, baada ya kupokea taarifa ya halmashauri hiyo juu ya mpango wake wa ujenzi wa soko jipya la kisasa.
Kinana ambaye alihimiza watendaji kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa masoko unakuwa shirikishi kuepuka migogoro na hasara, alisema wafanyabiashara wana uwezo wa kushauri ni muundo gani wa soko unawezesha kupata wateja. Baada ya kupokea taarifa hiyo ya halmashauri ikitaja mpango wake wa kujenga soko la ghorofa, Kinana alisema, "Mimi sijawahi kuona soko lenye ghorofa .
Nimezunguka nchi hii sana, Arusha, Tanga, Dar es Salaam nenda pale Kariakoo hakuna ghorofa." "Kwa nini nasema hivi? Kuna soko limeanzishwa Dar es Salaam linaitwa Machinga Complex, lina ghorofa mpaka juu sasa wameshindwa kulipa kodi.
Kwa sababu, nani yuko tayari kupanda ghorofa ya sita kwenda kununua chumvi...kwa nini asinunue chumvi barabarani kwa hiyo jihadharini," alisema.
Aliwaambia kwamba wanaweza kujenga ghorofa wakajikuta ghorofa ya juu haina mtu na ya chini ndiyo yenye watu wengi wakati huo huo madeni yakawa yamewakaba koo. "Halafu mnaanza kuwaambia wananchi tunapandisha kodi ili mlipe deni . Wanaolipa wananchi, waliokopa wakubwa. Hapana.
Changamsheni bongo ili wananchi wasiumie,” alishauri na kusisitiza ushirikishaji wa wafanyabiashara katika utekelezaji mpango huo. “Msiamue mambo wenyewe fuateni ushauri kutoka kwa wafanyabiashara watawaambia.
Nani anaweza kwenda kununua khanga ghorofa ya nne wakati barabarani ipo? Nani atakwenda kununua nyanya ghorofa ya pili wakati chini nyanya zipo?
Awali, katika risala ya wafanyabiashara wa Soko Kuu la Bukoba kupitia umoja wao, waliokuwa kwenye mvutano na halmashauri juu ya uamuzi wa kujenga soko hilo jipya, walisema hawapingi maendeleo bali wanaomba washirikishwe upatikanaji wa soko jipya kabla ya utekelezaji wa mpango huo

No comments:

Post a Comment