Wednesday, June 24, 2015

Mgomo mabasi wayeyuka


SERIKALI imekubaliana na umoja wa madereva katika madai yao waliyokuwa wakihitaji yatekelezwe, hali ambayo imemaliza tishio la kuwepo mgomo kwa mabasi yanayoenda mikoani pamoja na yale yanayofanya safari mijini.

Madai hayo ni pamoja na kupewa mikataba ya kudumu na waajiri wao, kukatiwa bima za afya pamoja kuongezewa mishahara.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichofikia makubaliano hayo, Katibu wa Umoja wa Madereva Nchini, Rashid Said alisema Serikali imekubali kusimamia na kutekeleza madai ya madereva ili kuepusha migomo ya mara kwa mara na kusababisha adha ya usafiri.
“Tumemaliza kikao chetu na mambo yote tuliyokuwa tunahitaji yatekelezwe yamekubalika. Lakini tumewaambia yatekelezwe ndani ya siku chache hizi na ifikapo Julai mosi mwaka huu kama hayajatekelezwa mgomo utakuwa pale pale,” alisema Said.
Alisema wamefurahishwa na maamuzi ya kikao hicho ambayo yatakuwa ni mkombozi wa maisha ya madereva, kwani kwa muda mrefu wamekuwa hawanufaiki na kazi yao zaidi ya kuwazalishia wamiliki kiasi kikubwa cha utajiri, lakini wao kubaki katika hali duni ya maisha.
Hivi karibuni madereva walitishia kuanzisha mgomo endapo Serikali haitayashughulikia madai yao ambayo kwa muda mrefu wamekuwa wakipiga kelele yatekelezwe.
Mgomo wa madereva nchini ulitokea mwanzoni mwa Mei mwaka huu na kudumu kwa siku mbili na kusababisha kero mbalimbali kwa wasafiri huku asilimia kubwa ya wananchi wakitembea wakati wakienda katika shughuli zao mbalimbali huku waliokuwa wakienda mikoani kukwama katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo.
Hata hivyo, mgomo huo ulisitishwa baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda Tume ya kushughulikia madai ya madereva ambayo hadi jana ilikuwa ikiendelea kujadiliana.

No comments:

Post a Comment