RAIS wa Marekani, Barack Obama anatarajiwa kuwa kiongozi wa tatu duniani kuanza kubeba kifimbo kama kile cha Mwalimu Nyerere ambacho tayari kimechongwa kwa ajili yake na msanii yule yule aliyetengeneza fimbo ya Baba wa Taifa.
Kiongozi wa pili kukabidhiwa ‘kifimbo cha uongozi,’ kama kile cha
Nyerere alikuwa ni Rais Jakaya Kikwete aliyepewa rasmi fimbo yake
mwishoni mwa wiki mjini Arusha, wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Kimataifa ya Albino Duniani iliyofanyika kitaifa mjini hapa. Kikwete
ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.
Kifimbo cha kwanza cha Mwalimu Nyerere kilichongwa mwanzoni kabisa
mwa miaka ya 1960 na mtaalamu wa sanaa za uchoraji, uchongaji na sayansi
za kitamaduni, Athuman Omari Mwariko, ambaye pia ndiye aliyeisanifu
ngao ya taifa pamoja na mwenge wa amani duniani.
“Nilimchongea tena Mwalimu Nyerere Kifimbo cha Pili mnamo mwaka 1985
kipindi kifupi tu kabla hajastaafu rasmi kutoka Ikulu,” anasema Mwariko
na inaonekana pia ameamua kuchonga kifimbo cha tatu na kumkabidhi Rais
Kikwete kabla kiongozi huyo hajang’atuka madarakani Oktoba mwaka huu.
Katika maisha yake yote, Mwaruko amechonga fimbo nne tu za uongozi na
waliobahatika kuvibeba vifimbo hivyo maalumu hadi sasa ni Baba wa
Taifa, Mwalimu Nyerere, Rais Jakaya Kikwete na hivi karibuni sasa
itakuwa ni Rais Barack Obama wa Marekani.
“Nimekwisha kupeleka ujumbe maalumu kwa Rais Obama pamoja na Ikulu ya
Marekani ili waandae siku na sehemu maalumu ambayo nitakwenda na
kumkabidhi rasmi kiongozi huyo fimbo maalumu ya uongozi,” alisema
Mwaruko ambaye pia amekuwa akiishi na kufanya kazi nchini Marekani kwa
miaka mingi.
Kuhusu fimbo ya Mwalimu Nyerere, Mwariko anasema; “Kila kiongozi ni
sharti awe na fimbo ya kuongozea,” anaongeza kuwa alimtengenezea Nyerere
fimbo yake ya kwanza wakati akianza uongozi miaka ya 1960 na baadaye
kumkabidhi fimbo ya pili wakati kiongozi huyo akistaafu urais mwaka
1985.
“Mimi ndiye nina siri ya mti uliotumika kuchongea fimbo hizo,”
anasema Mwariko na kuongeza kuwa fimbo zote za Mwalimu zilikuwa za
kawaida tu na wala hazina nguvu za ziada au miujiza kama watu
wanavyozusha.
Makazi yake nchini kwa sasa ni katika eneo la Njoro, katikati ya
Pasua na Majengo, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, akasema atakuwepo
hadi baada ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Mzee Mwariko alizaliwa mwaka 1949 eneo la Mbuyuni wilayani Moshi,
mkoani Kilimanjaro na alihudhuria masomo ya Msingi Handeni, Tanga na
baadae Moshi kabla ya kujiunga na Kings College ya Uganda na baadaye
Chuo Kikuu Cha Makerere nchini humo.
No comments:
Post a Comment