MILIO ya
risasi ilisikika katika vituo vya uandikishaji kura katika kata ya
Sokoni One jijini hapa, baada ya kuibuka kwa vurugu zilizohusisha vijana
wa Chadema na wenzao wa CCM, chanzo kikitajwa madai ya kuwepo kwa watu
ambao sio wakazi wa eneo hilo kutaka kujiandikisha.
Vurugu
hizo zilisababisha takribani watu 15 kukamatwa akiwemo Mbunge wa Jimbo
la Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ambaye hata hivyo baadaye
aliachiwa huru. Alishikiliwa kuanzia saa 1:30 usiku hadi saa 4:00 usiku
juzi.
Patashika
hiyo ilichukua zaidi ya saa moja, kwani baadhi ya polisi waliokuwa na
silaha za moto aina ya bastola walifyatua risasi hewani kwa lengo la
kutawanya vurugu hizo, lakini hali ilikuwa mbaya zaidi hadi polisi
walipoongezwa na kufanikiwa kutuliza ghasia hizo.
Wakati
hayo yanatokea Lema alisisitiza kuwa kamwe hawezi kukubali kutohamasisha
wananchi kwenda kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura
licha ya kudai kuwa, kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa wa CCM wamempiga
mawe sambamba na watu wengine waliojitokeza kujiandikisha katika kata
mbalimbali.
Hata
hivyo, upande wa vijana wa CCM, umedai wenzao wa Chadema ndio chanzo cha
vurugu, kwani wameonekana wakisambaza makundi ya vijana wasiostahili
kuandikisha katika vituo mbalimbali.
Lema
ajitetea Akizungumzia kukamatwa kwake na polisi wa kata ya Osunyai
kutokana na vurugu zilioibuka, alidai alikuwa akitoa taarifa za
uongezwaji wa mashine za BVR kwa wananchi na kuwapa moyo kuwa watulivu
wakati wa uandikishwaji sambamba na kutunza vitambulisho hivyo kwa ajili
ya kupiga kura mwaka huu katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na
madiwani.
Alisema
wakati akiendelea kuwapa moyo wananchi na kusema Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) imeongeza mashine za BVR, ghafla aliona vijana anaodai
wamekodishwa kufanya vurugu kwenye vituo mbalimbali vya kujindikisha na
ndipo alitoa taarifa Polisi, lakini badala ya kukamata vijana hao
alikamatwa yeye na vijana wengine na kuweka mahabusu.
NEC
iliruhusu uandikishaji kuendelea hadi saa mbili usiku kutokana na wingi
wa watu wanaostahili kuandikishwa. Hata hivyo mmoja wa wafuasi wa CCM
aliyejitambulisha kwa jina la Abdi Marijani maarufu kwa jina la ‘'Mutu’
alisema Chadema wamekuwa wakileta watu ambao sio wakazi Jiji la Arusha
kutaka kujiandikisha hali iliyopingwa na vijana hao.
Mutu
alisema CCM ilikuwa imepewa taarifa juu ya njama za Chadema za
uchomekeaji watu katika kila kata na chama kikaweka vijana imara katika
kila kituo wakiwa na mabalozi ambao ndio wenye jukumu la kujua mkazi wa
eneo husika.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa jana, Lema alisema juzi akiwa kata ya
Osunyai alishangaa kuona kundi la vijana wakiwa kwenye gari aina ya
Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 122 ATR ambalo alidai
wakati mwingine gari hilo lilibadilishwa namba na kusomeka T 122 ABR
wakishuka ghafla na kuanza kumpiga mawe na kuwapiga vijana wengine 25
ambao walikuwa katika kituo hicho.
Alisema
wakati tukio hilo likitokea alitoa taarifa kwa Mkuu wa Upelelezi wa
wilaya OC/CID, Faustine Mwafele ili kuwaelezea tukio hilo, lakini polisi
walifika eneo la tukio badala ya kuwakamata vijana hao walimkamata yeye
na vijana waliokuwepo kisha kuwaweka chini ya ulinzi.
Alisema
inaonekana kundi hilo linaonekana lipo juu ya sheria watu wanafanya fujo
za waziwazi, huku mbunge akigeuziwa 'na kusulubiwa.
Alisema
kwa kuwa yeye ni mbunge, hawezi kuacha kuhamasisha wananchi wake
kujiandikisha badala yake chama chao na viongozi wa chama wataendelea
kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha sambamba na kuhamasisha watu
wasikate tamaa katika kujiandikisha kwa sababu ni wajibu wao wa
kisheria, kisiasa na kidemokrasia.
Aliongeza
kuwa udhalilishwaji sasa umefika mwisho, hivyo alitoa rai kwa vijana wa
chama hicho kuchukua hatua ya kuwalinda viongozi wao, kulinda
demokrasia na mali zao.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana kuzungumzia tukio
hilo, licha ya kutafutwa kupitia simu yake ya mkono ikiwa ni pamoja na
kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi.
Wasemavyo
CCM Akizungumzia hilo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arusha, Feruz Banno
alisema vurugu zilianzishwa na vijana wa Chadema kwa kuwapiga vijana wa
CCM na kupiga risasi hewani hovyo bila ya sababu za msingi.
Banno
alisema dola Arusha inapaswa kuwa makini, kwani hali inaweza kuwa mbaya
zaidi iwapo hilo halitadhibitiwa na kuwafanya watu wengine kushindwa
kwenda kujiandikisha kwa kuogopa vurugu.
Alisema
kutokana na vurugu zinazofanywa kwenye baadhi ya vituo vya kujiandisha
na baadhi ya viongozi wa Chadema ili kudhibiti wazee na akinamama
wanaokwenda kujiandikisha kwenye vituo hivyo.
Alisema
kwa sasa uandikishaji unafanyika katika kata za Terati, Murieti,
Olusunyai, Moshono, Sinoni na Sokoni One, lakini baadhi ya vijana wa
chama hicho wamekuwa wakisafirishwa kwa magari kutoka kata tofauti na
hizo na kupelekwa eneo hilo kwa ajili ya kujiandikisha .
Ulinzi
Kwa upande wake Marijani, alisema kutokana na udhibiti uliowekwa na
makamanda wa CCM vituo vya kupigia kura wamebaini kuwa viongozi wa
Chadema na vijana wao wamekuwa wakileta vurugu katika kila kituo ili
zoezi hilo lisiweze kufanikiwa.
“Tumeweka
ulinzi kila kituo na hiyo itakuwa ikifanyika katika kata zote za Jiji
la Arusha kwani hiyo itasaidia kupata wakazi halisi wa eneo husika na
sio mamluki,” alisema Mutu.
No comments:
Post a Comment