Friday, April 17, 2015

Watanzania 64 waokolewa kwenye machafuko Yemen


Waziri wa Mambo ya Nje, Bernad Membe.
Waziri wa mambo ya nje Bernad Membe
SIKU chache baada ya kuwarudisha nchini Watanzania 25 kutoka Yemen, Serikali imetangaza kuwarudisha nyumbani Watanzania wengine 64 waliokuwa huko, ili kuwaepusha na machafuko yanayoendelea nchini humo.

Katika taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, serikali imefikia hatua hiyo ili kuwanusuru raia wake na machafuko nchini humo.
Taarifa hiyo ilisema Waziri wa wizara hiyo, Bernard Membe yuko nchino Oman kwa ziara ya siku moja na alizungumza na Balozi wa Tanzania nchini humo, Ali Ahmed Saleh, na kusema serikali ina jukumu la kuhakikisha usalama wa raia wake.
"Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye hatari na machafuko huko Yemen wanarejeshwa salama nyumbani mara moja," alisema Membe.
Alisema raia hao ambao wengi ni wanafunzi, watarejea nchini salama na hiyo ni kufuatia kupewa kwao ruhusu ya kuingia nchini Oman.
Na kuongeza, siku chache zilizopita, watanzania 25, walirudishwa nchini kutoka Yemen chini ya utaratibu wa Ofisi za Ubalozi wa Tanzania mjini Muscut,Oman, na sasa awamu hii watarudishwa raia 64.
Taarifa hiyo pia ilisema, hivi sasa wanafunzi hao wamefika kwenye mji wa Sarfat na Al-Mazyouna iliyopo mpakani mwa Oman na Yemen.
Katika taarifa hiyo, Membe alisema Watanzania hao ambao wengi wao hadi sasa wamefika miji ya Sarfat na Al-Mazyouna, walituma maombi ya dharura kwenye Ofisi za Ubalozi kuelezea mazingira ya hatari yanayowakabili, ambapo zoezi la kuhakiki, kuandikisha na kuwarudisha lilianza mara moja

No comments:

Post a Comment